Kuelekea Wiki ya Maji Dunia, WRBWB Yapanda Miti Pembezoni mwa Mto Mlali.

Kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Maji, WRBWB imeshirikiana na kikundi cha Jumuiya ya Watumia Maji Ngerengere Juu-A pamoja na Wananchi kupanda miti 300 aina ya Mikaranga katika chanzo cha Mto Mlali Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro.
Zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Sambamba na upandaji huo wa miti, wataalamu kutoka WRBWB wameendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi Rasilimali za Maji pamoja na Mazingira kwa ujumla.
Katika kuadhimisha Wiki ya Maji, Bodi imetoa ofa maalum kwa wananchi wenye visima ambapo watapatiwa huduma ya kupimiwa na kutibiwa maji bure bila gharama yoyote.
Hatua hiyo inalenga kuhamasisha jamii kuhakikisha maji wanayotumia ni salama kwa afya na yanatunzwa ipasavyo kwa maendeleo endelevu.
“Tone la maji lazima lihifadhiwe”



