EPUKA KUFANYA SHUGHULI ZA KIBINADAMU NDANI YA MITA 60 KUTOKA KWENYE VYANZO VYA MAJI.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu inaendelea na zoezi la kurejesha mito iliyopoteza mwelekeo wake katika njia yake ya asili kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala pamoja na wadau mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño.
Akizungumza kupitia Kituo cha Redio MUM FM 91.1 Morogoro Mhandisi. Joseph Kwitiga amesema hatua hiyo inaenda sambamba na kampeni endelevu ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Aidha amesema Wami/Ruvu imeendelea kuboresha vituo vya kupima na kufuatilia hali ya wingi wa maji hatua inayolenga kuongeza usahihi wa taarifa na utabiri wa ongezeko la maji katika mito.
Wami/Ruvu imewataka wananchi kuheshimu alama ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji kwa kuepuka shughuli za kilimo, ujenzi, uchimbaji wa madini na utupaji wa taka, ili kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha mito inaendelea kutiririsha maji kwa usalama.



