WANANCHI WATAKIWA KUTUNZA MAZINGIRA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI

Wananchi wametakiwa kuendelea kutunza mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukame unaojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani, ambapo amesisitiza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mtambule amesema kuwa uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti hovyo, uchimbaji wa mchanga usiofuata taratibu na utupaji holela wa taka unachangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi, hali inayosababisha upungufu wa mvua na maji katika maeneo mengi.
Ameonya kuwa uchimbaji wa mchanga usiozingatia sheria na kanuni za mazingira hautavumiliwa, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda mito, mabonde na vyanzo vya maji ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kunufaisha jamii kwa muda mrefu.
Aidha, amewahimiza wananchi kushiriki katika kampeni za upandaji miti kwa lengo la kuongeza uoto wa asili na kuifanya nchi kuwa ya kijani. Ameeleza kuwa kila wilaya inapaswa kuweka mikakati ya kupanda kati ya miti 1,500 hadi 3,000 kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kidakio vha Pwani, Bonde la Wami/Ruvu, Diana Kimbute, amesema Bodi inaendelea kutekeleza kampeni za usafi wa mito na mazingira ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kuhitimishwa Juni 5.
Katika hafla hiyo, washiriki wameshiriki mbio za afya (jogging) za umbali wa kilomita sita kama sehemu ya kuhamasisha afya bora, kuimarisha mshikamano wa jamii na kuendeleza ujumbe wa utunzaji wa mazingira.
Maadhimisho hayo yamewakutanisha viongozi, wadau wa mazingira na wananchi mbalimbali, ambao walionesha dhamira ya kushiriki kikamilifu katika shughuli zinazochangia ustawi wa jamii, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.




