Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba akagua Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba leo tar 02 Januari 2026 ameshuhudia kazi inayoendelea ya Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la maji Kidunda unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ndio suluhisho la changamoto ya upungufu wa Maji unaotokana na kukosekana na mvua kwa wakati katika Mto Ruvu ambao ndio chanzo tegemeo la wana Dar Es Salaam na Pwani.
Akiwa katika eneo la Mradi waziri Mkuu ameagiza Wizara ya Fedha kuupa kipaumbele mradi huu kwa kuhakikisha mkandarasi analipwa kwa wakati ili kazi ikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Lengo la ujenzi wa bwawa hili ni kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa matumizi ya majumbani, kilimo na shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro, Dar es salaam na Pwani hasa kipindi cha kiangazi.
Hali ya utekelezaji wa bwawa umefikia asilimia 40% na wasimamizi wa mradi pamoja na mkandarasi wamesisitizwa kuongeza kasi zaidi ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Ujenzi wa bwawa la Maji kidunda unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 336, na hadi sasa Serikali kupitia mapato yake ya ndani imeshamlipa mkandarasi kiasi cha takribani kiasi cha Billioni 100 ili kuwezesha utekelezaji wa mradi ambao unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa 2026.
Hivi sasa pamoja na kazi nyingine zinazoendelea, kazi kubwa inayokwenda kwa kasi ni ujenzi wa utoro na nyumba ya kuzalisha umeme yakiwa ni maandalizi ya kuchepusha mto kabla ya kipindi cha masika mwezi Machi 2026, hivyo kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa tuta litakalowezesha kuhifadhi maji lita billioni 190, zitakazotumika kwa ajili ya watu kwa matumizi ya majumbani hasa kipindi kina cha mto ruvu kinapopungua wakati wa ukame.
Aidha, mradi huu umesanifiwa pia kuzalisha umeme Megawat 20 kwa saa ambao utasafirishwa kutoka Kidunda kwenda kwenye gridi ya taifa Chalinze pamoja na matumizi ya umwagiliaji kwa shughuli za kilimo.



