DKT. NCHIMBI AIAGIZA WIZARA YA MAJI KUHIFADHI ARDHI OEVU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameagiza Wizara ya Maji kuhakikisha miradi yote ya maji nchini inatekelezwa kwa kuzingatia uhifadhi na ulinzi wa ardhi oevu ili kulinda mazingira na vyanzo vya maji.
Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo leo jijini Dodoma wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC).
Akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye yuko katika ziara ya kikazi nchini Urusi, Makamu wa Rais amesema ardhi oevu ni nguzo muhimu katika uhifadhi wa mazingira na uendelevu wa vyanzo vya maji nchini.
Amesema kuwa Tanzania inatarajiwa kuwa na zaidi ya wananchi milioni 100 ifikapo mwaka 2050, hali inayoongeza umuhimu wa kulinda ardhi oevu ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji, kupunguza changamoto ya upungufu wa maji na kuimarisha uhakika wa nishati kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, Makamu wa Rais ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha unakuwa na miche ya miti ya kutosha kwa ajili ya upandaji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji.
Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka kipaumbele katika masuala ya mazingira, ikiwemo uhifadhi wa ardhi oevu, ili kuhakikisha maendeleo endelevu yanakwenda sambamba na utunzaji wa rasilimali za asili.
Katika maelekezo mengine, Dkt. Nchimbi amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzisha na kutunza bustani za kijani katika maeneo yao kwa lengo la kuboresha mazingira na kuongeza mandhari ya kijani nchini.
Sambamba na hayo, Makamu wa Rais amezindua Programu ya Usimamizi wa Mazingira kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo itaanza kutekelezwa mwaka huu wa 2026 hadi mwaka 2030.
Maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Mazingira Duniani yamehitimishwa leo jijini Dodoma, yakitanguliwa na shughuli mbalimbali za kijamii na maonesho ya bidhaa na huduma kutoka taasisi, idara na vitengo vinavyoshiriki katika usimamizi, uhifadhi na ulinzi wa mazingira nchini.




