DIRA 2050
emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji
Bodi ya Maji Bonde la Wami/RUVU
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

 
Serikali kupitia Wizara ya Maji imetangaza kuendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maji, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Kidunda, lenye thamani ya shilingi bilioni 329.7, kwa lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na mikoa ya Pwani na Morogoro.
 
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maji 2026/2027 Bungeni, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 47, ni miongoni mwa miradi ya muda mrefu iliyokuwa ikisubiriwa kwa zaidi ya miongo sita, sasa umeanza kuleta matumaini mapya kwa wananchi.
 
Amesema tafiti mbalimbali za kihistoria, ikiwemo ya mwaka 1968, pamoja na ripoti za mashirika ya kimataifa kama Shirika la Kilimo na Chakula (1961), Shirika la Maendeleo la Ufaransa (1962), Japan (1962) na Norway (2005), zote zilithibitisha umuhimu wa kujengwa kwa bwawa hilo kama suluhisho la kudumu la tatizo la maji Dar es Salaam.
 
Aweso ameeleza kuwa licha ya usanifu wa mradi kukamilika mwaka 2014, utekelezaji wake haukuanza hadi Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonesha dhamira ya dhati kwa kuanza ujenzi wa bwawa hilo kwa kutumia fedha za ndani.
 
“Bwawa la Kidunda ambalo kwa miaka mingi lilikuwa kwenye makaratasi, sasa linajengwa kwa vitendo. Huu ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua changamoto za wananchi,” amesema Aweso.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutahakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika katika majimbo 18 ya Dar es Salaam, ikiwemo Ilala, Segerea, Ukonga, Temeke, Kigamboni, Ubungo na Kinondoni, pamoja na maeneo ya Pwani na Morogoro, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
 
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa urahisi, huku akisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni kielelezo cha vitendo vya Serikali katika kuboresha maisha ya Watanzania.

Mpangilio

slot gacor