MHA. MWAJUMA AITAKA TIMU YA MRADI WA BONDE DOGO LA MTO MKONDOA KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ameshiriki kikao cha kwanza cha Kamati ya Uendeshaji wa Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika Rasilimali za Maji katika Bonde Dogo la Mto Mkondoa.
Akizungumza kwa njia ya simu katika kikao hicho Mhandisi Mwajuma amewataka wataalamu na wadau wote wanaohusika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa ili kuepusha changamoto zinazoweza kuchelewesha au kukwamisha utekelezaji wake.
Amesema utekelezaji mzuri wa mradi huo utasaidia kuimarisha upatikanaji na usimamizi wa rasilimali za maji jambo litakalowanufaisha wananchi wa sasa pamoja na vizazi vijavyo.
Aidha Mhandisi Mwajuma amesema Bonde la Wami/Ruvu ni miongoni mwa mabonde muhimu ya maji yanayotoa huduma kwa wananchi likitegemewa kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa maji katika maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Kwa msingi huo amesisitiza umuhimu wa timu inayosimamia mradi huo kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na uwajibikaji ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati na kuongeza nguvu katika upatikanaji wa maji ya kutosha na salama.
Kwa upande wake Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imeeleza kuwa itaendelea kushiriki kikamilifu katika uratibu na utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia misingi ya weledi, uwazi, uwajibikaji na kuzingatia matokeo.
Mradi huo umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na unatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2026 hadi 2029, ukiwa na gharama ya Dola za Marekani 14,024,196.



