Tahadhari ya Mafuriko Kuanzia 26 FEB. hadi 03 MACHI 2026.

Taarifa ya utabiri wa mafuriko unaonesha Kuna uwezekano wa wastani wa kutokea kwa mafuriko katika kipindi cha kuanzia tarehe 26 Februari hadi 3 Machi, 2026 katika baadhi ya maeneo yaliyopo ndani ya Bonde la Wami/Ruvu, hususani katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.
Kwa mujibu wa utabiri umebainisha baadhi ya maeneo yanayotarajiwa kukumbwa na mafuriko ambayo ni Kijiji cha Kibaoni, Masanze, Malui, Munisagara, Tindiga, Magomeni-Kilosa, Kisala na Kijiji cha Kilimanjaro, hivyo Bodi inatoa wito kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuchukua tahadhari ili kujilinda na athari zinazoweza kujitokeza.
Aidha, mamlaka husika zinasisitizwa kuondoa vizuizi vya maji katika madaraja ili kuruhusu mtiririko sahihi wa maji na kupunguza hatari ya mafuriko.
Bodi itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa viwango vya mitiririko ya maji na kutoa taarifa zaidi.
“Tone la maji lazima lihifadhiwe “



