ZOEZI LA UPIMAJI WA UBORA WA MAJI YA VISIMA BILA MALIPO LAENDELEA MOROGORO.

Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu inaendelea na Maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa kaulimbiu ya “Maji na Jinsia”, kwa kutekeleza shughuli mbalimbali zinazolenga utunzaji na uhifadhi wa rasilimali za maji katika Manispaa ya Morogoro.
Katika Kuadhimisha Wiki Maji Bodi Imejikita katika Utoaji wa Huduma Maalum kwa Wananchi ikiwemo Upimaji wa Ubora wa Maji ya Visima, Utoaji wa Ushauri wa Kitaalamu kuhusu Matumizi sahihi ya Maji pamoja na njia Bora za Kuhifadhi Rasilimali hii Muhimu.
Aidha Visima vitakavyobainika kuwa na Uchafuzi wa vimelea (bakteria) vitapatiwa Huduma ya Matibabu ya Maji bila malipo.
Huduma hizi zinatolewa katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro ikiwemo kata za Mkundi, Chamwino, Kichangani, Lukobe, Kidunda na Mafisa, ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na fursa hii Muhimu.
Sambamba na hilo Bodi imefungua kituo Maalum cha kupokea na kushughulikia Kero za Wananchi zinazohusiana na Masuala ya Ubora wa Maji.
Kituo hicho kinapatikana katika Banda la Bodi lililopo Stendi ya Zamani ya Mkoa wa Morogoro Wananchi wote wanahimizwa kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizi muhimu pamoja na kushiriki kikamilifu katika jitihada za kulinda na kuhifadhi Rasilimali za Maji kwa maendeleo endelevu ya jamii.



