WAZIRI AWESO AAGIZA RASILIMALI ZA MAJI ZITUMIKE KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA HUDUMA YA MAJISAFI NA SALAMA.

Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso amezitaka taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji kutumia ipasavyo rasilimali za maji zilizopo nchini ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi katika kila kijiji kwa lengo la kutimiza maelekezo na dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Aweso ametoa wito huo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji; Bi. Rose Zacharia Ambrose ambapo amesisitiza kuwa mito na vyanzo vingine vya maji ni rasilimali muhimu zinazopaswa kutumika kikamilifu katika uzalishaji wa maji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani waliopo vijijini na maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji.
Aidha, Mhe. Aweso amebainisha mwelekeo wa Wizara ni kuhamia katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upokeaji, uchakataji na utoaji wa taarifa, pamoja na kuboresha uwajibikaji na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso ameitaka Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kufanya tathmini ya chanzo cha maji chini ya ardhi katika eneo la Kimbiji sambamba na kufanya uchambuzi wa shughuli za kibinaadamu zenye athari kwa mikondo ya maji lengo likiwa ni kuongeza hali ya upatikanaji wa majisafi katika Jiji la Dar es Salaam.



