Waziri Aweso amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji (National Water Grid), unaolenga kuunganisha vyanzo vikuu vya maji ikiwemo maziwa, mito mikubwa na mabwawa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote ya nchi.
Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo, Aweso amesema katika utekelezaji huo, Wizara imekamilisha usanifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida, huku ikiendelea na usanifu wa miradi ya maji kutoka Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, pamoja na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kupeleka Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.




