WAZIRI ULEGA AWATAKA WAHANDISI KUTOA SULUHISHO ZA KITAALAMU KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NINO.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imeshiriki Mkutano wa Mwaka wa Wahandisi uliofanyika leo, Septemba 24, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kujadili masuala ya uhandisi na mchango wa wataalamu hao katika kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika mkutano huo akiwa Mgeni Rasmi, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Hamis Ulega, amewataka wahandisi nchini kutumia utaalamu, ubunifu na teknolojia katika kuandaa suluhisho za kitaalamu za kukabiliana na changamoto za kimazingira, ikiwemo athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño na mafuriko.
“Hivi karibuni tunatarajia mvua za El Nino. Tunaomba Mungu zisizidi uwezo, lakini wahandisi mna jukumu la kuhakikisha mnaonesha njia na suluhisho jinsi ya kuepuka majanga kama mafuriko na kadhalika,” amesema Waziri Ulega.
Aidha, Waziri Ulega amesema Serikali inatarajia mvua za El Niño na kuwataka wahandisi kuonesha njia na kutoa suluhisho la kitaalamu litakalosaidia kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, hususan mafuriko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kuwapa wahandisi nafasi ya kushiriki katika masuala ya ulinzi wa mazingira kupitia shughuli zao za kila siku ili maendeleo yaende sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Ushiriki wa Wami/Ruvu katika mkutano huo unaimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya uhandisi katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za maji na mazingira, pamoja na kuendeleza matumizi ya utaalamu wa kihandisi katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.



