emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji
Bodi ya Maji Bonde la Wami/RUVU
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

Wizara ya Maji imefanya kikao cha pamoja na wawakilishi kutoka World Waternet, WRBWB pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA).
Kikao hicho kimejikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo, hususan katika masuala ya uhifadhi wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, ikiwemo Bwawa la Mindu ambalo ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro. Aidha, kikao kimeweka msisitizo katika kupanga mikakati ya utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu wa Mashirikiano (2027–2030).
 
Kupitia ushirikiano huo, juhudi mbalimbali zimeendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kulinda vyanzo vya maji dhidi ya uharibifu wa mazingira, kudhibiti mmomonyoko wa ardhi, kupunguza upotevu wa maji (NRW), pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za maji.
 
Mradi wa uhifadhi wa Bwawa la Mindu una umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa upatikanaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Morogoro, kwani unasaidia kuhakikisha uwepo wa maji ya kutosha na salama kwa matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.
Aidha, juhudi hizi zinachangia kupunguza changamoto ya upungufu wa maji, kuimarisha mifumo ya usambazaji, na kuongeza uendelevu wa huduma ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini.
 
Kwa ujumla, ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuhakikisha rasilimali za maji zinalindwa na kutumika kwa ufanisi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa Morogoro.

Mpangilio