Gridi ya Maji ya Taifa Kupunguza Uhaba wa Maji Nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Maji Bw. Hussein Ally, amesema mpango uliopo wa Wizara ya Maji kuanzisha Gridi ya Maji ya Taifa unalenga kufikisha maji kwenye maeneo yenye uhaba wa maji, kwa kutumia maji kutoka maeneo yenye wingi.
Mwenyekiti ameyasema hayo kwenye kipindi cha Mizani cha TBC1, akisisitiza umuhimu wa uhifadhi, utunzaji na uendelezaji wa rasilimali za maji ili kuimarisha usalama wa maji kwa vizazi vijavyo, akitolea mfano mpango endelevu wa Wizara wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria na kuyafikisha maeneo ya katikati ya nchi, ambapo mpaka sasa mradi huo umefikia wilayani Nzega, mkoani Tabora.
Mpango huo amesema ni sehemu ya jitihada za Wizara kuhakikisha usambazaji wa maji unafikiwa kwa usawa kote nchini, na kupunguza tofauti ya upatikanaji wa maji kati ya vijiji, miji midogo na mijini.
Mwenyekiti ameeleza kuwa mpango huu ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu ya Wizara ya Maji ya kuhakikisha rasilimali za maji zinatunzwa na kusambazwa kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na Bodi za Maji za Mabonde, Jumuiya za Watumiaji wa Maji, pamoja na sekta binafsi ili kufanikisha malengo hayo.
Aidha, amesema Wizara hiyo ina mipango mingine ya kuhakikisha maji yanapatikana na kuhifadhiwa kwa matumizi ya kila Mtanzania, ikiwemo maendeleo ya miundombinu ya mabomba, mabwawa madogo na mikondo ya maji ili kuongeza ufanisi wa usambazaji wa maji nchini.



