OTESHA yawasilisha wazo la mradi wa matumizi ya teknolojia katika uhifadhi wa mazingira, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na urejeshwaji wa maeneo yenye uharibifu.

Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu imepokea ugeni kutoka kampuni ya OTESHA kwa ajili ya kuwasilisha na kujadili mradi wao wa maendeleo unaolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia, uhifadhi wa mazingira na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji.
Katika kikao hicho, OTESHA iliwasilisha wazo la mradi unaohusisha matumizi ya teknolojia katika kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na urejeshwaji wa maeneo yenye uharibifu wa kimazingira.
Aidha, kikao hicho kililenga kujadili fursa za ushirikiano kati ya Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu na Otesha katika utekelezaji wa miradi yenye tija, ikiwemo kuendeleza ubunifu, kuimarisha ushiriki wa jamii na kuchochea maendeleo endelevu katika sekta ya maji.
Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza jukumu la kulinda, kuhifadhi na kusimamia rasilimali za maji kwa manufaa ya jamii na vizazi vijavyo.




