Kamati ya Bunge yaipongeza Wami/Ruvu kwa Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imepongeza juhudi za Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu katika ujenzi wa mradi wa birika la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Sangasanga, Kitongoji cha Masanze na Lubungo, Wilaya ya Morogoro, unaolenga kulinda vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu.
Pongezi hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Patrick Mwalunenge (Mb), wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, huku akiwataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Amesema upatikanaji wa huduma ya maji kwa mifugo katika maeneo maalumu ni hatua muhimu katika kupunguza athari za shughuli za ufugaji zinazofanyika ndani na pembezoni mwa vyanzo vya maji, hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo vizuri na kuhakikisha miundombinu iliyojengwa inatunzwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy amesema mradi huo umejengwa kwa lengo la kupunguza athari za mifugo katika vyanzo vya maji vya Mto Mlali na Bwawa la Mindu, kwa kuwezesha mifugo kupata huduma ya maji katika eneo maalumu badala ya kuingia moja kwa moja kwenye vyanzo hivyo.
Amebainisha kuwa mradi unatekelezwa na wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo World Waternet umegharimu shilingi milioni 65, huku ukihusisha uchimbaji wa kisima chenye urefu wa mita 110, ufungaji wa mfumo wa nishati ya jua, ujenzi wa mnara wa tenki la maji pamoja na mtandao wa mabomba wenye urefu wa mita 54.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Sangasanga wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika miradi ya maji inayolenga kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha shughuli za ufugaji na kulinda mazingira.
Wamesema mradi huo utawasaidia kupata huduma ya maji kwa urahisi zaidi, kupunguza changamoto za mifugo kutafuta maji katika vyanzo vya asili na kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji katika matumizi ya rasilimali za maji.



