Wami/Ruvu yamafanya usafi katika Mto Morogoro.

Kuelekea Katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu na wadau mbalimbali wakiwemo waosha magari wamafanya usafi katika Mto Morogoro pamoja na kutoa elimu ya mazingira kwa jamii na wanafunzi wa shule mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhandisi Mazingira Abdallah Mshana, ametoa wito kwa wananchi kuacha kufanya shughuli zinazohatarisha vyanzo vya maji na kuzingatia kanuni za uhifadhi wa mazingira.
“Vyanzo vya maji ni uhai wa jamii. Tunapaswa kuvihifadhi kwa kuepuka utupaji holela wa taka, uvamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji na shughuli nyingine zinazochangia uharibifu wa mazingira,” amesema Mshana.
Sambamba na hilo, Bodi imeendelea kutoa elimu ya mazingira katika shule mbalimbali ikiwemo Shule za Sekondari Konga na Kauzeni, kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uelewa na kuwahamasisha kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira katika jamii zao.
Kwa upande wake, mshiriki wa zoezi hilo Kurwa Chamlungu amesema ushiriki wa taasisi mbalimbali katika shughuli za mazingira unaongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.
Naye mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Konga, Angela Michael, amewahimiza vijana na wanafunzi kujiunga na Klabu za Mazingira zilizoanzishwa na Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu ili kushiriki katika kampeni za usafi, utoaji wa elimu na mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira.




