emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji
Bodi ya Maji Bonde la Wami/RUVU
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

 
Kuelekea katika Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayotarajiwa kufanyika mwezi Machi, WRBWB imeitisha jukwaa la wadau wa Kidakio cha Ngerengere kwa lengo la kuimarisha usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Jukwaa hilo limekuwa sehemu ya maandalizi ya kitaasisi ya kuadhimisha Wiki ya Maji, yenye kaulimbiu ya “Maji na Jinsia”, inayosisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia katika usimamizi na upatikanaji wa rasilimali za maji.
Aidha jukwaa hilo limewahusisha Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa pamoja na wawakilishi kutoka MORUWASA, NEMC, TFS, Ofisi ya Mkoa, Halmashauri za Wilaya, viwanda na Jumuiya za Watumia Maji.
Katika kikao hicho, wadau walipewa elimu kuhusu sheria na miongozo ya usimamizi wa rasilimali za maji, umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji pamoja na kuimarisha ushiriki wa jamii. Aidha, walipata nafasi ya kujadili miradi inayotekelezwa katika Kidakio cha Ngerengere, mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazoathiri uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Jukwaa hilo limefanyika kwa ushirikiano na International Union for Conservation of Nature (IUCN), likilenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, sekta binafsi na jamii katika kulinda rasilimali za maji.
Kupitia jukwaa hilo, Bodi imehimiza wadau kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za Wiki ya Maji na kuchukua hatua madhubuti za kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa sasa na vizazi vijavyo.

Mpangilio