WADAU WATATHIMINI UTEKELEZAJI WA MRADI WA UHIFADHI BWAWA LA MINDU, WAPANGA MABORESHO YA AWAMU YA PILI.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), World Waternet na Shirika la Kilimo Endelevu (SAT) imefanya kikao kazi cha kutathmini utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mradi wa Uhifadhi wa Bwawa la Mindu.
Kikao hicho kimelenga kupitia maendeleo yaliyofikiwa, kutambua mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi katika eneo la mfano la Mto Ngerengere, ambalo ni moja ya vyanzo muhimu vinavyochangia maji katika Bwawa la Mindu.
Washiriki wa kikao wamejadili kwa kina hatua mbalimbali zilizotekelezwa katika kipindi cha awamu ya kwanza na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za kuimarisha uhifadhi wa Rasilimali za Maji na mazingira katika eneo la Mradi.
Aidha kikao kimetoa fursa ya kuandaa mpango wa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi kwa kuweka vipaumbele na mapendekezo yatakayoboresha utekelezaji wa shughuli za uhifadhi, Awamu hiyo inatarajiwa kupanua wigo wa shughuli za uhifadhi katika mito mingine inayochangia maji yanayoingia katika Bwawa la Mindu.
Wadau wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za serikali, washirika wa maendeleo na jamii zinazozunguka maeneo ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinakuwa endelevu na zinachangia upatikanaji wa maji ya uhakika kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro na maeneo jirani.
Mradi wa Uhifadhi wa Bwawa la Mindu unalenga kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi mazingira ya bonde la maji na kuimarisha usalama wa upatikanaji wa maji kwa kizazi cha sasa na kijacho kupitia usimamizi endelevu wa Rasilimali za Maji.




