Taarifa ya Hali ya Wingi wa Maji katika Mto Ruvu

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imeandaa na kuwasilisha Taarifa ya Hali ya Wingi wa Maji katika Mto Ruvu, ikionesha kuwa wingi wa maji katika mto unatarajiwa kuendelea kuongezeka na kubaki juu ya wastani katika kipindi cha kuanzia Septemba 15 hadi 25, 2026.
Taarifa hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mwenendo wa maji katika vituo vilivyopo ndani ya kidakio cha Ruvu, pamoja na utabiri wa hali ya mvua na joto uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Kwa sasa, Mto Ruvu una wingi wa maji unaofikia takribani lita 12,120 kwa sekunde, wakati mahitaji ya maji yanakadiriwa kuwa karibu lita 6,000 kwa sekunde hali hiyo inatarajiwa kuwa himilivu katika kipindi cha siku kumi zijazo na kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji ya maji katika sekta mbalimbali.
Aidha Ongezeko la maji katika Mto Ruvu linachangiwa na mvua zilizonyesha katika Safu za Milima ya Uluguru, ambazo ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayochangia maji katika Mto Ruvu, Maji ya Mto Ruvu ni muhimu kwa matumizi ya majumbani yanayohudumiwa na mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, pamoja na shughuli za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ujenzi, Madini, Viwanda na Utalii.
Bodi inawataka watumiaji wa maji kuendelea kutumia rasilimali hiyo kwa ufanisi na kuzingatia matumizi endelevu, ikiwemo Mamlaka na Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira.
Hatahivyo Bodi itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa wingi wa maji katika Mto Ruvu na kutoa taarifa kila baada ya siku kumi, ili kuwafikishia wadau taarifa sahihi na za wakati kuhusu hali ya upatikanaji wa maji na kuwawezesha kupanga matumizi yao kwa wakati.



