TAKWIMU ZA KITAALAMU ZAONESHA KUIMARIKA KWA AKIBA YA MAJI CHINI YA ARDHI KIMBIJI.

Bodi ya maji, Bonde la Wami/Ruvu katika jitihada za kuendelea kusimamia rasilimali za maji kwa ufanisi, zoezi la ufuatiliaji wa mwenendo wa maji chini ya ardhi limefanyika katika visima vikubwa vilivyopo eneo la Chanika- Kimbiji
Kupitia uchukuaji wa takwimu katika visima vya EB2 na EB3, imebainika kuwa kina cha maji kimeongezeka kwa mita 0.6.
Ongezeko hili, kwa mtazamo wa kitaalamu wa Hydrogeologia linaashiria uwepo wa uwiano mzuri kati ya ujazo wa maji unaoingia ardhini (recharge) na ule unaotumika (discharge), hali inayodhihirisha uthabiti wa akiba ya maji chini ya ardhi (aquifer).
Mwenendo huu chanya unaonesha kuwa mfumo wa ikolojia unaozunguka eneo hilo bado una uwezo wa kuruhusu maji ya mvua kupenya ardhini na kujaza vyanzo vya maji, jambo linalochangiwa na uhifadhi wa mazingira na matumizi sahihi ya ardhi.
Matokeo haya yanatoa dira na matumaini kwa upatikanaji endelevu wa maji huku yakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mikakati ya kisayansi katika usimamizi wa rasilimali za maji.
Wananchi wanahimizwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, kupunguza uharibifu wa vyanzo vya maji na kutumia maji kwa uangalifu ili kulinda mafanikio haya kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.



