KAMATI YA KIDAKIO CHA WAMI YAPITIA UTEKELEZAJI WA MPANGO KAZI, YAJIWEKEA MIKAKATI YA MWAKA WA FEDHA 2026/2027.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kupitia Kamati ya Maji ya Kidakio cha Wami, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Hamza Sadiki, imefanya Kikao cha Pili cha Kamati hiyo kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na kujadili na kupitisha Mpango Kazi wa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kikao hicho, kimewakutanisha wajumbe wa Kamati ya Maji ya Kidakio cha Wami ambapo wamepitia kwa kina taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizotekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo Wajumbe wamejadili mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa shughuli hizo, ikiwemo hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji ndani ya kidakio hicho, pamoja na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu hayo.
Katika majadiliano hayo, wajumbe wametoa maoni pamoja na mapendekezo yenye lengo la kuimarisha utekelezaji wa shughuli za Kamati, Mapendekezo hayo yanatarajiwa kusaidia kutatua changamoto zilizobainika, kuboresha utendaji wa Kamati, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za maji na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wanaohusika na usimamizi wa vyanzo vya maji.
Aidha, kikao hicho kimepitia na kujadili Mpango Kazi wa mwaka wa fedha 2026/2027, ambapo wajumbe wametoa michango mbalimbali inayolenga kuboresha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kwa mwaka ujao wa fedha.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli, kupanga mikakati ya kuboresha utendaji wa Kamati ya Maji ya Kidakio cha Wami na kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.




