WAMI/RUVU, TRC WAWEKA MFUMO WA TAHADHARI YA MAFURIKO KWA TEKNOLOJIA YA RADA

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kupitia Kidakio Maji cha Kinyasungwe kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC), imekamilisha vituo viwili vya ufuatiliaji wa kiwango cha maji kwa teknolojia ya rada, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa taarifa za maji kwa wakati halisi na utoaji wa tahadhari mapema katika maeneo ya miundombinu ya reli.
Vituo hivyo vilivyopo Mbori–Matomondo na Kinyasungwe–Kongwa ni sehemu ya vituo vitatu vinavyojengwa, huku ujenzi wa kituo cha Mtanana–Kibaigwa ukiendelea. Mfumo huo hupima kiwango cha maji bila kugusa maji na kutuma taarifa moja kwa moja kwenye mifumo ya kidijitali ya Wami/Ruvu na TRC.
Taarifa hizo zitawezesha kufuatilia mabadiliko ya viwango vya maji kwa wakati, kuchukua hatua za haraka pale hatari ya mafuriko inapojitokeza na kuimarisha ulinzi wa reli dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na kuongezeka kwa maji.
Hatua hiyo pia inaongeza matumizi ya teknolojia na takwimu katika usimamizi wa rasilimali za maji, huku ikiimarisha ushirikiano wa Wami/Ruvu na TRC katika kulinda miundombinu muhimu ya Taifa.



