Wami/Ruvu Yaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa Kupanda Miti na Kutoa Elimu kwa Wananchi Mvomero.

Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani 2026 Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imefanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira katika Wilaya ya Mvomero.
Miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni utoaji wa elimu ya mazingira kwa wanafunzi na wananchi pamoja na upandaji wa miti katika Shule ya Sekondari Nasoro, Vilevile wadau hao wameshiriki katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika Mto Kisengele uliopo Kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.
Wakizungumza baada ya shughuli hizo wananchi wametoa shukrani zao kwa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika shughuli za usafi wa mazingira.
Pia Wananchi hao wameeleza kuwa elimu iliyotolewa imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za maji huku wakiahidi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.




