Wami/Ruvu Yaendelea Kuelimisha Umma Kuhusu Uhifadhi wa Vyanzo vya Maji na Taratibu za Matumizi ya Rasilimali za Maji.

Leo tarehe 8 Julai 2026 Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imefanya mahojiano maalum kupitia kituo cha redio MUM FM cha Morogoro ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu usimamizi endelevu wa rasilimali za maji na uhifadhi wa mazingira.
Katika mahojiano hayo, wataalamu wa Bodi wamesisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji pamoja na mazingira yanayovichangia ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha na salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha wananchi wameelimishwa kuhusu taratibu za kupata vibali vya matumizi ya maji na vibali vya utupaji wa majitaka kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia usimamizi wa Rasilimali za Maji nchini.
Sambamba na hilo wataalamu wameeleza kwa kina hatua za awali hadi za mwisho za maendeleo ya mradi wa uchimbaji wa maji chini ya ardhi ikiwemo utafiti wa kitaalamu, uchimbaji wa kisima, upimaji wa ubora na wingi wa maji pamoja na taratibu za kuhakikisha maji yanayopatikana ni safi, salama na yanakidhi viwango vinavyoruhusiwa kwa matumizi ya Binadamu.
Wami/Ruvu imewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda vyanzo vya maji kuzingatia matumizi endelevu ya rasilimali za maji na kufuata taratibu zote za kisheria ili kuhakikisha Rasilimali hiyo muhimu inaendelea kupatikana kwa manufaa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
#Tonelamajilazimalihifadhiwe




