WATUMISHI WAMI/RUVU WAJADILI UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TAASISI.

Watumishi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kutoka katika vidakio vya Wami, Ruvu, Ngerengere pamoja na Kinyasungwe Mkoa wa Dodoma leo Mei 18, 2026 wamekutana katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika Makao Makuu ya ofisi za Bodi ya Wami/Ruvu hiyo Mkoani Morogoro.
Kikao hicho kimelenga kujadili utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya taasisi kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na mipango ya utekelezaji wa kazi kwa mwezi Juni 2026, Washiriki kutoka vitengo na vidakio mbalimbali wamewasilisha taarifa za utekelezaji wa shughuli zao pamoja na mipango ya maendeleo ya taasisi.
Katika kikao hicho Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy, ametoa maelekezo na mtazamo wa taasisi kwa mwaka 2026/2027 huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ushirikiano na kuendelea kufanya kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya taasisi.
Aidha kikao hicho kimejadili masuala ya uadilifu sambamba na tunu pamoja na maadili ya Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Watumishi pia wamepata nafasi ya kuwasilisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili katika mazingira ya kazi kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na ustawi wa watumishi.
Vilevile Mhandisi Mmassy amekabidhi vifaa vya huduma ya kwanza (First Aid Kits) kwa madereva wa taasisi pamoja na vidakio vyote vya Bodi hiyo ili kuimarisha usalama na huduma za dharura mahali pa kazi.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa maazimio mbalimbali yaliyolenga kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za maji ndani ya Bonde la Wami/Ruvu.



