WAMI/RUVU YAUNDA JUMUIYA ZA WATUMIA MAJI RUVU CHINI.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya maji pamoja na serikali za kata na vijiji vinavyopakana na Mto Ruvu katika wilaya za Kibaha na Bagamoyo imeendesha zoezi la kuunda Jumuiya za Watumia Maji Ruvu Chini kwa lengo la kuimarisha usimamizi shirikishi na endelevu wa rasilimali za maji.
Zoezi hilo limehusisha makundi mbalimbali ya watumia maji ikiwemo viwanda kupitia Chama cha Viwanda (KEDA), vyama vya wafugaji, vyama vya wakulima, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia mtambo wa Ruvu Juu, pamoja na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kupitia CBWSO ya UKIKI iliyopo Kata ya Vigwaza.
Wakizungumza wataalamu kutoka Wami/Ruvu wameeleza umuhimu wa jumuiya za watumia na lengo kuu la kuanzishwa kwa Jumuiya hizi ni kuhakikisha usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji, kulinda mazingira yanayozunguka hifadhi za mito pamoja na kuimarisha matumizi endelevu ya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika utekelezaji wa zoezi hili jumla ya vijiji 17 vimepatiwa elimu kuhusu usimamizi wa Rasilimali za Maji na kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kuunda Jumuiya za Watumia Maji, Hatua hii inalenga kuweka msingi wa usimamizi wa pamoja, kuongeza uwajibikaji wa wadau na kuhakikisha usawa katika utunzaji na ulinzi wa vyanzo vya maji.
Wami/Ruvu imewataka wananchi, taasisi na wadau wote wanaotegemea Mto Ruvu kuendelea kushiriki katika juhudi za kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu unaendelea kuwa endelevu kwa jamii na shughuli za kiuchumi zinazotegemea maji hayo.




