WAMI/RUVU YAKAGUA MIFUMO YA KUTIBU MAJITAKA VIWANDANI KABLA YA KUTOA VIBALI VYA UTIRIRISHAJI, KUIMARISHA ULINZI WA VYANZO VYA MAJI NA MAZINGIRA.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imefanya ukaguzi wa mifumo ya kutibu majitaka katika kiwanda cha Watercom kilichopo Kisarawe II, Wilaya ya Kigamboni na kiwanda cha TPLCLC kilichopo Kata ya Wazo, Wilaya ya Kinondoni.
Ukaguzi huo umelenga kutathmini utendaji, ufanisi na uwezo wa mifumo iliyowekwa na viwanda hivyo katika kutibu majitaka kabla ya kutolewa kwa vibali vya utiririshaji. Hatua hiyo inahakikisha kuwa majitaka yanayotokana na shughuli za uzalishaji viwandani yanatibiwa ipasavyo na kukidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuruhusiwa kutiririshwa katika mazingira.
Kupitia ukaguzi huo, Bodi ya Maji inaendelea kuhakikisha kuwa viwanda vinawajibika ipasavyo katika usimamizi wa majitaka yanayotokana na shughuli zao kwa kuzingatia matakwa ya kisheria na masharti ya vibali. Aidha, Bodi inahimiza wawekezaji na wamiliki wa viwanda kuwekeza katika mifumo bora na yenye ufanisi ya kutibu majitaka ili kuzuia uchafuzi wa mito, vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.



