WAMI/RUVU, MORUWASA NA WORLD WATERNET WAKAMILISHA VIKAO VYA SIKU TANO, WAANDAA AWAMU YA TATU YA MIRADI YA MAJI MOROGORO.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na MORUWASA pamoja na World Waternet Leo Aprili 24, 2026 Wamekamilisha vikao vya Majumuisho vilivyodumu kwa siku tano vikilenga kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ushirikiano huo.
Katika vikao hivyo wadau wamepitia kwa kina taarifa za utekelezaji wa Miradi kwa awamu ya pili huku wakitathmini mafanikio, changamoto na masomo yaliyopatikana.
Aidha wameandaa mpango kazi madhubuti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za awamu ya tatu ya miradi hiyo.
Makubaliano yaliyofikiwa katika awamu ya tatu Bonde la Wami/Ruvu itatekeleza shughuli mbalimbali katika eneo la Mto Mlali, Shughuli hizo zitajumuisha Uanzishaji wa Mashamba Darasa ya kilimo Msitu, Uandaaji wa Vitalu vya Miti, pamoja na hatua nyingine za kuhifadhi Mazingira na Vyanzo vya Maji.
Sambamba na hilo kupitia majadiliano na National Water Fund na Tanga UWASA wadau hao wanatarajia kuanzisha Mfuko wa Maji kwa Mkoa wa Morogoro.
Mfuko huo unalenga kuunganisha wadau mbalimbali ili kuchangia juhudi za uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa mkoa Morogoro.
Hatua hii inatarajiwa kuimarisha usimamizi endelevu wa Rasilimali za Maji na kuongeza upatikanaji wa huduma bora ya maji kwa jamii.
"Tonelamajilazimalihifadhiwe"



