WAMI/RUVU YASHIRIKI ZIARA YA WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA KUKAGUA USAFI WA MTO NG’OMBE

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imeshiriki ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Makamu wa Rais kuhusu usafishaji na uhifadhi wa Mto Ng’ombe, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na El Niño.
Waziri amekagua eneo lenye urefu wa takribani kilomita tano kuzunguka Daraja la Mto Ng’ombe, Tandale na Kijitonyama, katika Manispaa ya Kinondoni. Ameliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Kinondoni, kukamilisha ndani ya wiki moja sehemu iliyobaki ya usafishaji wa mto huo. Pia, amezitaka Ofisi za Mazingira kuimarisha usimamizi wa mazingira na kusisitiza kuwa taka zinaweza kuwa fursa za kiuchumi kwa kurejeleza taka badala ya kuzitupa kwenye mito. Ameeleza kuwa atarejea kukagua maeneo ya Mto Ng’ombe na Ghoba.
Meneja wa Mazingira wa Wami/Ruvu, Bi. Janeth Kisoma, amewahimiza wananchi kuacha uchafuzi wa vyanzo vya maji kama vile kutupa taka ngumu na kutiririsha majitaka kwenye Mito. “Kulinda mito ni kulinda maisha yetu. Taka zina thamani, lakini mito ikichafuliwa, madhara yanaturudia sisi wenyewe!” amesema.



