WAMI-RUVU YATOA ELIMU YA UHIFADHI WA MAZINGIRA KWA WASHIRIKI WA COP-12

Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kwa washiriki kutoka mataifa mbalimbali wanaoshiriki katika Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umeanza Oktoba 6 na unatarajiwa kuendelea hadi Oktoba 9, 2026, ukiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kujadili masuala yanayohusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Mkataba wa Nairobi (Nairobi Convention) ni mkataba wa kimataifa unaolenga kuimarisha hifadhi, usimamizi na uendelezaji endelevu wa mazingira ya bahari na ukanda wa pwani wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Bodi ya Maji Bonde la Wami-Ruvu, ikiwa ni miongoni mwa wadau wanaoshiriki katika mkutano huo, imetumia fursa hiyo kutoa elimu kwa washiriki kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za maji.
Kupitia ushiriki wake katika COP12, Bodi hiyo inaendelea kuhamasisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu wajibu wa pamoja katika uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



