WAMI/RUVU WATOA ELIMU KUHUSU UWEKAJI WA MIPAKA YA MAKATAZO.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) imefanya kikao cha uelimishaji kwa wananchi wa mitaa ya Mundu na Kilala kuhusu zoezi la uwekaji wa Mipaka ya Makatazo kando ya Mto Mzinga.
Lengo la kikao hicho ni kuwajengea wananchi uelewa kuhusu umuhimu wa uwekaji wa mipaka ya makatazo itakayowekwa pembezoni mwa Mto Mzinga, pamoja na kueleza namna zoezi hilo litakavyotekelezwa.
Katika kikao hicho wananchi wameelimishwa kuwa kazi ya uwekaji wa alama hizo za kudumu inatarajiwa kuanza mwezi Julai 2026, Zoezi hilo linalenga kuhifadhi na kulinda hifadhi ya mita 60 kutoka kingo za Mto Mzinga kwa kuzingatia sheria na miongozo ya usimamizi endelevu wa Rasilimali za Maji.
Uwekaji wa mipaka ya makatazo unatarajiwa kusaidia kuzuia uvamizi wa maeneo ya hifadhi ya mto, kulinda mazingira, kuboresha usimamizi wa Rasilimali za Maji na kuhakikisha Mto Mzinga unaendelea kuwa chanzo salama na endelevu cha maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wami/Ruvu imewataka wananchi kuendelea kushirikiana wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kufanikisha juhudi za uhifadhi na ulinzi wa mazingira ya Mto Mzinga.
Tonelamajilazimalihifadhiwe




