WAMI/RUVU YAIMARISHA UHIFADHI WA RASILIMALI ZA MAJI KUPITIA TATHMINI NA UKAGUZI WA MITO.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imeendelea kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji kwa kufanya tathmini na ukaguzi wa mito mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji na ulinzi wa mazingira.
Tathmini hiyo imekuja kufuatia ongezeko la mashapo yanayosababishwa na uharibifu wa vyanzo vya maji, uchimbaji holela wa mchanga, utupaji wa taka, kilimo kisichozingatia sheria, ujenzi usioruhusiwa na uondoaji wa uoto wa asili kandokando ya mito, hali inayohatarisha mtiririko wa maji.
Wataalamu wa Wami/Ruvu wamekagua mito ya Msimbazi, Tegeta, Mbezi, Mpiji na Mkuza ili kubaini kiwango cha mashapo, uharibifu wa kingo za mito na athari zake. Matokeo ya ukaguzi huo yatasaidia kupanga hatua za kitaalamu za urejeshaji na usimamizi endelevu wa mito.
Bodi ya Maji imeonya dhidi ya shughuli zote zinazofanyika ndani ya mito au vyanzo vya maji bila vibali halali, ikisisitiza kuwa wanaokiuka masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, Sura ya 331 (Toleo la Marekebisho la 2023), watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, Wami/Ruvu inatoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi mazingira na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohatarisha rasilimali za maji, kwa kuwa ushirikiano wa jamii ni msingi wa kuhakikisha maji yanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.




