WAMI/RUVU YAIMARISHA UTAMBUZI WA WATUMIAJI MAJI KIKUYU KUSINI.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imeendelea na zoezi la utambuzi wa watumiaji wa maji katika Kata ya Kikuyu Kusini, likiwafikia wananchi wa Mitaa ya Mkuyuni na Magorofani, ikiwa ni hatua ya kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali maji.
Kupitia zoezi hilo, Bodi inawafikia wananchi moja kwa moja na kutoa elimu kuhusu taratibu za matumizi ya maji, ikiwemo umuhimu wa kuwa na vibali kwa matumizi yanayohitaji kibali, pamoja na kuzingatia masharti ya usimamizi wa rasilimali maji.
Wananchi pia wanaelimishwa kuhusu madhara ya uchimbaji holela wa visima na umuhimu wa kutumia rasilimali maji chini ya ardhi kwa kuzingatia taratibu, huku taarifa za watumiaji zikisaidia Bodi kufahamu mahitaji na matumizi ya maji katika maeneo husika.
Zoezi hilo pia lina umuhimu katika kujiandaa na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa katika kipindi cha El Niño, ambapo taarifa sahihi za watumiaji na matumizi ya maji zitasaidia kuimarisha ufuatiliaji, tahadhari na usimamizi wa rasilimali maji.



