WAMI RUVU YAWAONYA WANAOCHIMBA VISIMA BILA VIBALI.

Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imewaonya wananchi na taasisi zinazochimba visima bila kufuata taratibu za kisheria kuwa zinakabiliwa na faini isiyopungua Shilingi milioni saba au kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa rasilimali za maji.
Onyo hilo limetolewa na Afisa Mazingira Bw. Rajabu Mwinyialipo wakati wa kikao cha utoaji elimu kwa watumia maji kilichofanyika Tarafa ya Hombolo, Wilaya ya Dodoma, kikihusisha viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa rasilimali za maji na taratibu za utoaji wa vibali vya matumizi ya maji.
Katika kikao hicho, washiriki walikumbushwa umuhimu wa kupata vibali kabla ya kuchimba visima au kutumia maji kutoka vyanzo mbalimbali, huku wamiliki wa visima wakitakiwa kuhakikisha visima vyao vinasajiliwa katika Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Maji (UMIS), bila kujali kama ni vya matumizi ya nyumbani au miradi mikubwa ya usambazaji maji.
Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu imeeleza kuwa itaendelea kutoa elimu kwa jamii na kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha matumizi ya rasilimali za maji yanafanyika kwa kuzingatia sheria, kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha huduma hiyo muhimu inapatikana kwa njia endelevu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.



