WRBWB YASHEREHEKEA SIKU YA KUMBUKIZI YA KUZALIWA MHE. RAIS SSH KWA KUPANDA MITI, MVOVERO

Bodi kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Mvomero pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, wamefanikisha zoezi la upandaji wa miti zaidi ya 250 katika chanzo cha maji cha Mto Mahululu.
Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 27-01-2026, kama ishara ya kuenzi juhudi zake katika kulinda mazingira na rasilimali maji.
Akiongoza zoezi hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mvomero, Saidi Nguya, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, ametoa wito kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa vyanzo vya maji kuacha shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo, hatua itakayosaidia kulinda vyanzo vya maji na kuepuka changamoto ya upungufu wa maji kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Magreth Phat, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kidakio cha Wami kutoka, ameushukuru uongozi wa Wilaya ya Mvomero pamoja na wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika utunzaji wa vyanzo vya maji kama njia ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, akibainisha kuwa ulinzi wa vyanzo vya maji ni jukumu la kila mmoja.
Naye Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Mvomero, Medison Nilahi, amewasihi wananchi kutumia vyema kipindi cha masika kupanda miti, huku akisisitiza kuwa TFS ipo tayari kugawa miche ya miti bure kwa wananchi ili kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira.
Wananchi wameipongeza Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu kwa zoezi hilo na kuahidi kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.



