WRBWB Yazindua Zoezi la Kupima & Kutibu Visima bila Malipo.

Kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Maji Duniani, WRBWB leo Machi 10, 2026 imezindua rasmi zoezi la Upimaji na Kutibu Ubora wa Maji ya Visima bila malipo kwa Wananchi wa Manispaa ya Morogoro pamoja na maeneo yote yaliyo ndani ya mipaka ya Usimamizi wa Bonde la Wami/Ruvu.
Uzinduzi wa zoezi hili Umefanywa na Mhe. Musa Kilakala Mkuu wa Wilaya ya Morogoro katika Hafla iliyohudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani 39, Watendaji wa Kata 29, Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa, Afisa Tarafa pamoja na Meya wa Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza Wakati wa Uzinduzi huo Mhe. Kilakala amewataka Wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro kutumia kikamilifu fursa hiyo Muhimu ili waweze kufahamu Ubora wa Maji ya Visima wanayotumia kila siku na kuhakikisha kuwa yanakidhi viwango vya Usalama na Afya kwa Matumizi ya Binadamu.
Aidha ameeleza kuwa zoezi hili litasaidia kubaini changamoto zinazoweza kuwepo katika Ubora wa Maji ya Visima na kutoa hatua stahiki za kitaalamu ili kuhakikisha wananchi wanatumia maji safi na salama.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi; Mhandisi Elibariki Mmassy, amesema kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, Bodi imeanzisha zoezi maalum la kutibu maji ili kuhakikisha yanaendelea kuwa safi na salama kwa matumizi ya wananchi.
Ameongeza kuwa huduma hiyo itatolewa bila malipo kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vyeti vinavyothibitisha ubora wa maji kutoka kwenye visima, ili kuwapa wananchi uhakika wa usalama wa maji wanayotumia wakati wote.
Zoezi hili linatarajiwa kuwafikia Wananchi wengi katika maeneo mbalimbali Morogoro na kanda nzima ya Bonde la Wami/Ruvu huku wataalamu wa maji wakiendelea kutoa huduma za Upimaji na Ushauri wa Kitaalamu kuhusu namna bora ya kuhifadhi na kutumia Maji ya Visima kwa Usalama.
“Tonelamajilazimalihifadhiwe”



