emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maji
Bodi ya Maji Bonde la Wami/RUVU
ega Logo
Habari
ega-svg-tree

WRBWB imepanda miti 500 rafiki kwa maji pamoja na miti ya matunda katika eneo la Mto Msimbazi uliopo Mtaa wa Mogo, Kata ya Kipawa, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Wiki ya Maji.
Zoezi limeongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa John Mrema, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kinyerezi. Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na Mwenyekiti wa WRBWB Nickson Lutenda, Diwani wa Kata ya Kipawa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mogo, Kamati ya Mazingira ya Mogo pamoja na wakandarasi na machepe wanaofanya shughuli za kusafisha Mto Msimbazi.
 
Lengo ni kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, kulinda kingo za mito na kukumbusha umuhimu wa kupanda na kutunza miti kwa ajili ya ustawi wa mazingira na upatikanaji endelevu wa Rasilimali za Maji.
Akizungumza wakati wa zoezi, Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam amehimiza wananchi kuendelea kulinda na kutunza miti iliyopandwa ili kusaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na kulinda mazingira ya mito.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WRBWB amewataka wananchi wenye mifugo kutumia maeneo mbadala ya malisho badala ya kupeleka mifugo kandokando ya mito kwani hali hiyo husababisha uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Amesisitiza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za Bodi ya Maji kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutumia rasilimali za maji kwa uendelevu.
 
Bodi ya Maji inatoa wito kwa wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kupanda miti, kuepuka shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi ya mito pamoja na kuzingatia sheria na taratibu za usimamizi wa rasilimali za maji kwa manufaa yetu sote.

Mpangilio